Afisa Tawala, Ofisi ya Waziri Mkuu, Leah Kibassa, akifanya mazoezi ya kutumia kizima moto wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa watumishi wa Ofisi hiyo, mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brig. Jen. Mbazi Msuya (mwenye tai) akishuhudia, Salma Juma akikabidhiwa Kizima moto kilichonunuliwa na washiriki wa mafunzo ya menejimenti ya maafa wa Ofisi hiyo mjini Dodoma tarehe, 21 Juni, 2015, Kwa lengo la kuhamasisha watumishi wa Ofisi hiyo kukabili majanga ya moto.
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mafunzo ya majanga ya moto wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa mjini Dodoma.
………………………………………………………
Na. Mwandishi Maalum
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa inaandaa mkakati wa elimu kwa umma wa menejimenti ya maafa ambao utawatumia watu maarufu nchini wakiwemo wasanii wa sanaa mbali mbali kwa lengo la kufikisha elimu kwa umma ya menejimenti ya maafa.
Akiongea wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki hii, Brig.Jen, Mbazi Msuya alibainisha kuwa jamii ikielimishwa kikamilifu juu ya menejimenti ya maafa athari za maafa zinapunguzika.
“Tunaposema menejimenti ya maafa tunazingatia, kuzuia, kukabili maafa na kurejesha hali ya awali baada ya maafa kutokea. Kwa mantiki hii kama tunavyo elewa Wasanii wanao uwezo wa kufikisha ujumbe kwa haraka, lugha nyepesi, kwa watu wengi na kwa ujumbe mmoja, hili ndo linalotusukuma kufikiria kutumia hawa watu katika kutoa elimu ya menejimenti ya maafa kwa jamii yetu” alisema Msuya.
Msuya aliongeza kuwa nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga ya asili na yale yanayosababishwa na binadamu, ambapo majanga yanayosababishwa na binadamu kwa kiwango kikubwa jamii inaweza kuyakabili tu ikiwa elimu ya menejimenti ya maafa hayo imemfikia kila mwanachi. Hivyo kwa kuwa wasanii wengi msingi wa kazi zao za sanaa huaksi yanayojiri katika jamii yao hivyo hii itakuwa ni fursa kwao kuijengea jamii uwezo wa kuyakabili maafa.
“Athari za Majanga yanayosababishwa na binadamu kama moto yanaweza kuzuilika ikiwa menejimenti ya majanga hayo itatolewa kwa umma. Wananchi wakielimishwa umuhimu wa kuwa na vizima moto majumbani mwao na katika vyombo vya moto wanaweza kukabili majanga ya moto na hili litawezekana kwani tayari tunayo mikakati ya mawasiliano ya kukabiliana na maafa ” alisisitiza Msuya.
Ofisi ya waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu maafa tayari imeshaandaa Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara, Shinyanga na Dodoma lengo ikiwa ni kila mkoa nchini kuwa na mkakati huo utakowezesha menejimenti ya maafa kwa jamii ya watanzania. Aidha mkakati huo unabainisha kila mdau wa maafa wajibu wake katika menejimenti ya maafa wakiwemo wasanii.
0 comments :
Post a Comment