Mbunge Joshua Nassar akiwa na mkewe Anande Nnko wakati wa sherehe ya kimila iliyoandaliwa na wananchi katika jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kufanikiwa kumaliza mgogoro wa maji uliokuwepo katika baadhi ya vijiji .
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii KAnda ya Kaskazini.
WANANCHI wa vijiji vya Leguruki na King’ori katika wilaya ya Arumeru wameandaa sherehe kubwa kwa ajili ya mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki ,Joshua Nassar baada ya kutatua mgogoro wa maji uliodumu kwa muda mrefu katika vijiji 15 vya wilaya hiyo.
Sherehe hiyo iliyoenda sanjari na shughuli za kimila ilishuhudiwa mbunge huyo pamoja na mkewe Anande Nnko wakivishwa maazi ya kimila pamoja na kukabidhiwa rungu huku mkewe akikabidhiwa kibuyu pamoja na ijiti cha kimila.
Uamuzi wa wananchi hao unatokana na Mbunge Joshua Nassar kutatua mgogoro kwa kuunda timu ya viongozi wa Din,Mila,Vijiji na kuamua kuwapeleka Dodoma na kukutana na Waziri wa maji,Waziri wa Tamisemi na Waziri wa Nishati na Madini kwa ajili ya mazungumzo.
Safari ya viongozi hao ndio iliyozaa kuvunjwa kwa iliyojiita bodi ya maji yaliyofadhiliwa na shirika la OIKOS East Africa kwa vijiji 15 katika wilaya hiyo huku ikiwalipisha wananchi kwa lita.
Mbali na kutozwa fedha kwa wananchi hayo bodi hiyo pia ilidaiwa kusababisha baadhi ya wananchi kuwekwa rumande kwa hila huku mbunge huyo akipambana na kufanikiwa kuwatoa.
Katika sherehe hiyo viongozi wa mila na dini walimsimika Nassar huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkno katika mapambano ya kupigania wananchi wa Meru ili kuondokana na hali ya umaskini.
Akizungumza katika hotuba yake ,Nassar alisema bodi ya maji imevunjwa na kauli ya waziri wa maji ni "wananchi ndio wenye Mamlaka ya mwisho kimaamuzi.
“Linapokuja swala la namna bora ya kuchangia na sio kulipia, ikizingatiwa mradi huu ulijengwa kwa nguvu za wananchi bila malipo yeyote kwa miaka 3 wananchi wanapaswa kupata huduma hii ya maji”alisema Nassar.
Nassar alitumia sherehe hiyo kukabidhi magari ya kubeba wagonjwa huku yakiombewa na kuwekwa wakfu ili yakawe sehemu ya uponyaji kwa watu wa Arumeru Mashariki.
Wananchi wamekiri kwa umoja wao "hawajawahi kupata Mbunge Kama Nassari baada ya Japhet Kirilo.
Mwisho.
|
0 comments :
Post a Comment