Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodgrigues, akiwasilisha mada katika warsha ya siku tatu iliyofanyika katika kijiji cha Nyakahungwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza kuhusu ushirikishaji jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayochangia kuzuia na kutokomeza unyanyasaji na dhulma zinazofanywa dhidi ya watu wenye albinism iliyoshirikisha waganga wa asili, wauguzi na wakunga, viongozi wa dini, walimu pamoja na watu maarufu iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).
...................................................................................................................................
Na Modewjiblog team, Mwanza.
Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) yanayoendelea nchini yanatokana na mitazamo hasi kitamaduni miongoni mwa wanajamii.
Hayo yameelezwa na washiriki wa warsha ya siku tatu inayoendelea katika kijiji cha Nyakahungwa kata ya Nyakahungwa wilayani Sengerema yenye lengo la kubadili mitazamo iliyojengeka katika jamii na kusababisha madhara makubwa kwa watu wenye albinism iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Warsha hiyo ni miongoni mwa mlolongo wa warsha nne zitakazofanyika katika wilaya za Sengerema, Mwanza, Kahama na Bariadi kwa kuzishirikisha jamii kuibua masuala mbalimbali yanayobagua, kunyanyapaa na kuwatenga watu wenye albinism katika maeneo husika.
Warsha hizo zinafanyika katika kipindi ambacho kumetokea mauaji ya mtoto wa kike, msichana na kijana wenye albinism wilayani Sengerema wakati tarehe 14 Mei 2015 mwanamke mmoja alikatwa mkono wilayani Bariadi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Sengerema, Bw. Bushaija Vicent (kulia), akitoa takwimu za idadi ya za wanafunzi wenye albinism katika wilaya yake kwa Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO Bi. Zulmira Rodgrigues.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo Jamii wilayani Sengerema Bwana Bushaija Vicent kati ya shule za msingi 191 wilayani humo ni Shule zenye watoto wenye albinism ni 14, Idadi yao ni 16 katika shule ya awali watoto 4 wana albinisim, vyuo mbalimbali Sengerema vijana 4 wana albinism na katika Shule za sekondari 48, watoto wenye albinism 4.
Akitoa mada kuhusu uhamasishaji jamii katika masuala ya albinism, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO Bi Zulmira Rodgrigues amesema miongoni mwa masuala ambayo warsha italenga ni kutafakari kwa kina kwa nini watu wenye albinism wanauawa, kubaguliwa, kutengwa na mambo yanayosababisha Tanzania kuongoza katika mauaji hayo ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo pia zina watu wenye albinism.
“Watu wenye albinism hawauwawi katika sehemu nyingine duniani, kwa nini Tanzania? Ikiwa mauaji hayo yako kwa wingi nchini Tanzania basi kuna tatizo kubwa ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi, na si serikali, UNESCO wala taasisi yoyote ambayo inaweza kuleta mabadiliko hayo isipokuwa jamii yenyewe,” alisema Rodrigues.
Tatizo kubwa lililotajwa kuhusiana na mauaji ya watu wenye albinism ni utamaduni uliojengeka katika fikra za watu na kuwa na imani kwamba watu wenye albinism si watu wa kawaida, hawana hadhi na hawastahili kuishi.
Watu wenye albinism ni watu wa kawaida wanaostahili heshima na kulindwa kama binadamu wengine kulingana na kanuni na sheria za nchi na za kimataifa zinazopinga ubaguzi wa rangi, jinsia, tabaka na kukatisha maisha ya mtu. Tofauti ni kwamba rangi yao inatokana na ukosefu wa vinasaba asili vijulikanavyo kama melanin, vyenye uwezo wa kuzalisha rangi ya nywele, macho na ngozi.
Utamaduni uliojengeka katika jamii wa kuwabagua, kuwatenga na kuwapuuza watu wenye ulemavu wa ngozi kumehalalisha mauaji ambayo kwa hivi sasa imekuwa biashara ya kuuza viungo vya watu wenye albinism kwa waganga wa asili kwa lengo la kupata utajiri, cheo na madaraka.
“Mara nyingi waganga wa asili wamekuwa wakitajwa kuwa ndio chanzo cha mauaji hayo kwa ajili ya imani potofu ya kujipatia utajiri, vyeo na madaraka. Biashara hiyo inaonekana kushamiri kwa kuwa hakuna mifumo mahsusi kudhibiti maafa hayo,” alisema mmoja wa washiriki anayeshughulikia masuala ya usalama.
Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO Bi. Rose Haji Mwalimu, akichangia mada kuhusu ushirikishaji jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayochangia kuzuia na kutokomeza unyanyasaji na dhulma zinazofanywa dhidi ya watu wenye albinism iliyoshirikisha waganga wa asili, wauguzi na wakunga, viongozi wa dini, walimu pamoja na watu maarufu iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Katikati ni Mratibu ambaye pia ni Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias na Kulia ni Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodgrigues.
Akichangia mada wakati wa majadiliano yanayokusudiwa kuzalisha mikakati ya kukomesha maovu hayo, Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO Bi Rose Haji Mwalimu alisema kwamba wakati umefika wa kutambua kitu gani kizuri katika tamaduni zilizopo zitakazoweza kusaidia kuleta mafanikio na kuachana na zile ambazo hazina tija na zinasababisha maafa katika maendeleo na ustawi wa jamii.
“Ni kweli kuna changamoto nyingi katika jamii zinazosababishwa na kuhalalisha tamaduni zinazolenga kupotosha badala ya kujenga. Tukiendelea kuzikumbatia tutajikuta tunajenga taifa lisiloona mbali kimaendeleo kuhadaiwa na watu wenye ubinafsi kutoka nje na ndio maana Tanzania imekuwa soko kubwa au shamba lenye rutuba ya kupandikiza mbegu ambazo mavuno yake hupatikana kwa urahisi”, alisema Bi Mwalimu.
Katika warsha hiyo washiriki walibaini maeneo makuu matatu ya kuyawekea mpango kazi. Maeneo hayo ni Kuzuia mauaji, ubaguzi, unyanyapaa na kuwatenga, eneo la pili ni kuwalinda watu wenye albinism katika maeneo ya makazi, mashuleni, katika jamii na familia zao na la tatu ni hatua za kisheria wale wote watakaoonekana kuhusika moja kwa moja au kwa namna nyingine katika kuwatendea maovu watu wenye ulemavu wa ngozi kuanzia ngazi za kimataifa, kitaifa, kifamilia na shuleni.
Mganga wa jadi kutoka kijiji Nyanzenda, wilayani Sengerema, Maimuna Musa akizungumzia jinsi anavyotoa huduma za kutibu watoto magonjwa mbalimbali ya watoto ikiwemo na huduma ya kuzuia mwanamke asizae mtoto mwenye ulemavu wa ngozi.
Mganga wa jadi kutoka kijiji cha Nyakasungwa, Omary Mongongwa akitoa msimamo kuhusu uwezo wa tiba kwa waganga wa jadi unavyotofautiana na kuwasihi waganga wenzake wa jadi wanapojadili wazungumzie kazi za mtu binafsi na utendaji wake na si kuusemea moyo wa mganga mwingine.
Mzee maarufu kutoka kijiji cha Bukokwa, Felician Buhumbi, akifafanua hatua zilizokuwa zikichukuliwa wakati wa Ukoloni dhidi ya waganga asili wenye kupiga ramli chonganishi wakati wa warsha ya siku tatu iliyofanyika katika kijiji cha Nyakahungwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo ya siku tatu iliyowashirikisha, Waganga wa Jadi, Viongozi wa dini, walimu shule za msingi na sekondari, wazee maarufu, Wakunga, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Shirika la Under the Same Sun, Baraza la taifa la dawa asilia, Afisa wa polisi wa dawati la jinsia pamoja na Maafisa wa mkoa wa Mwanza na wa wilaya ya Sengerema.
Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodgrigues aliyeambatana na mbunge wa viti maalum CCM anayetetea maslahi ya watu wenye albinism, Mh. Al-Shaymaa Kwegyir wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki.
0 comments :
Post a Comment