UZINDUZI WA KAMPENI ZA KUPINGA NDOA ZA UTOTONI WAFANYIKA JIJINI DSM.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe akizungumza katika uzinduzi wa kampeni maalumu za kitaifa za kupinga ndoa za utotoni (National Ending Child Marriage Campaign), zitakazo endeshwa Mkoani Mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka (kwanza kulia) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni maalumu za kitaifa za kupinga ndoa za utotoni (National Ending Child Marriage Campaign), zitakazo endeshwa Mkoani Mara. Kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi nchini (UNHCR), Bi. Joyce Mendez Kole.


Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi nchini (UNHCR), Bi. Joyce Mendez Kole akizungumza katika hafla hiyo. Kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Dk. Natalia Kanem.

Kutoka kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa UN Women nchini Tanzania, Anna Collins, Meneja wa Haki za Watoto kutoka Graca Michel Trust, Bernard Orimbo na mwakilishi wa asasi za Mkoa wa Mara.

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na mashirika na asasi anuai zinazotetea haki za watoto na jamii kwa ujumla imezinduwa kampeni maalumu za kitaifa za kupinga ndoa za utotoni (National Ending Child Marriage Campaign) ambazo zimekuwa zikikwamisha haki ya elimu kwa mtoto wa kike. 

Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaan kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Shirika lisilo la Kiserikali la Children’s Dignity Forum (CDF), Graca Machel Trust (GMT), asasi za mkoani Mara na uongozi wa mkoa huo. 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe alisema Serikali ipo kwenye mchakato wa kupitia sheria zake ikiwemo Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ambayo imekuwa na utata juu ya umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike. 
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, pamoja na mambo mengine inaruhusu mtoto wa kike miaka 14 au 15, kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au mahakama jambo ambalo linatajwa na wanaharakati kuwa kikwazo cha elimu kwa mtoto huyo. 

Akifafanua zaidi Katibu Mkuu aliwahakikishia washiriki wa mkutano huo kuwa sheria hiyo itabadilika hasa baada ya mchakato wa katiba kukamilika hivyo kuwataka wananchi kwa kushirikiana na asasi anuai kuunga mkono juhudi za kupinga ndoa za utotoni zinazoendekezwa kwa baadhi ya maeneo nchini Tanzania. 

Alisema uwepo wa udhaifu wa sheria isiwe kisingizio cha kuendeleza vitendo hivyo viovu kwenye jamii kwani Serikali wakati wote kupitia watendaji wake ipo tayari kupambana na watu wanaoendeleza vitendo hivyo pale inapofikishiwa taarifa. 

“…Jamii lazima ikubali kubadilika na kuacha vitendo hivi vya kuwaozesha watoto, hivi kati yetu hapa nani anakubali mtoto wake akatishwe masomo na kuozeshwa? Tukiwa tayari kupiga vita kuanzia kwenye familia zetu makazi yetu suala hili litakoma…Ni kweli Serikali ipo kwenye utaratibu wa kuipitia sheria na nawahakikishia itafanyiwa mabadiliko lakini kama jamii nasi tunatakiwa kubadilika na kuacha vitendo hivi,” alisema Bi. Maembe.

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka alisema shughuli za kampeni hizo maalumu za kupinga ndoa za utotoni zinatarajiwa kufanyika Mkoani Mara na zitaambatana na utoaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, watendaji wa vyombo vinavyosimamia sheria, 
viongozi wa jamii na jamii kwa ujumla juu ya mapambano ya kampeni hizo. Alisema kampeni hizo baadaye zitaendelea katika maeneo mengine ya Tanzania lakini kwa sasa Mkoa wa Mara ndipo zitakapoanzia na limechukuliwa kama eneo la mfano kwa kuanzia.
 “Tunaamini tunaweza kushirikiana na jamii kwa kuwalinda watoto wetu ambao wamekuwa wakinyimwa haki ya msingi ya kupata elimu na baadhi ya watu,” alisema Bi. Nsoka. 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Children’s Dignity Forum (CDF), Koshuma Mtengeti akizungumza katika hafla hiyo alisema takwimu zinaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo inaidadi kubwa ya ndoa za utotoni. 

Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kati ya wasichana 5 wanaoolewa Tanzania wawili kati yao huolewa wakiwa chini ya miaka 18 ilhali sheria ikiendelea kuwa na utata. 
 
Aidha Meneja wa Haki za Watoto kutoka Graca Michel Trust, Bernard Orimbo juhudi za makusudi zikifanywa kwa makundi yote kampeni hizo zinaweza kufanikiwa kwani taasisi hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Zambia ilipata mafanikio makubwa dhidi ya kampeni kama hizo zilizoanza kufanyika mwaka 2013.

Imeandaliwa na www.thehabari.com

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment