Mali imesema inapanga kuwashitaki wazazi ambao wanawasafirisha watoto wao wadogo kwenda Ulaya kama wahamiaji, lakini kufanya hivyo kutahitaji ushirikiano na Ulaya.
Waziri katika serikali ya Mali ameiambia BBC kuwa familia zinaongezeka zinazowatuma watoto kwenda Ulaya kupitia mazingira magumu kama vile uvukaji wa bahari.
Wanafanya hivyo kwa sababu watoto wakifika huko hawafukuzwi.
Abderrahmane Sylla ameyaomba mataifa ya Ulaya kuwatambua watoto wanaosafiri peke yao ili kuisaidia serikali ya Mali kupambana na wazazi wanaofanya hivyo.
Amesema ana matumaini kuwa hatua ya kuwashitaki itasaidia kuwazuia wazazi kufanya hivyo.
Bwana Sylla, ambaye ni waziri wa wananchi wa Mali waishio nje ya nchi, amesema anapata karibu kila siku taarifa za vifo vya wananchi wa Mali katika bahari ya Mediterani.
Ametolea mfano wa boti iliyokuwa imejaa abiria ambayo iliondoka Libya mwezi Julai ikiwa na raia 87 wa Mali miongoni mwa abiria hao 86 walikufa, 17 wakiwa wanatoka kijiji kimoja.
Bwana Sylla amesema wizara yake imeandaa rasimu ya sheria ambayo itawasilishwa bungeni baada ya hivi karibuni kurejea kutoka safari katika kisiwa cha Lampedusa, nchini Italia, ambako aliwaona watoto wawili wa Mali wenye umri wa miaka 10 na 12, na kumfanya kuchukua hatua hiyo.
"Hali hii ilinitoa machozi... Watoto hawa wanapita njia ile ile wanayopita watu wazima - Ouagadougou, Niger, Chad, Libya; halafu wanakabiliana na safari ngumu ya majini kama ilivyo kwa wakubwa.," alisema.
"Kwa hiyo wanafika pwani ya Ulaya wakiwa na kiwewe. Tunatakiwa kuwaadhibu wanaowatuma watoto wao katika safari hizi hatari; tunatakiwa kukomesha hili."
Bwana Sylla amesema wnanchi wa Mali wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza nchi na kukomesha tabia ya uhamiaji.
Source BBC Swahil.
0 comments :
Post a Comment