TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania waishio nje ya nchi na wanaotaka kuona Tanzania inakubali kuanzisha mfumo wa uraia pacha kutumia muda wao kujenga hoja za jambo hilo badala ya kupoteza muda kwenye mijadala ya blogu na kulaumi watu wengine.
Rais Kikwete amewataka Watanzania hao kusema ili wasikike kwa sababu, kimsingi, hoja ya uraia pacha haina nguvu miongoni mwa Watanzania wanaoishi Tanzania bali hoja hii inatokana zaidi na msukumo wa Watanzania wanaoishi nje ambao kwa bahati mbaya hawafanyi jitihada za kutosha kutetea hoja yao.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipokutana, akazungumza na kujibu maswali ya Watanzania wanaoishi Marekani, hasa katika maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya Virginia, Maryland, New York na hata California katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tisa katika Marekani ambako miongoni mwa mambo mengine atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Marekani na Afrika ambao shughuli zake zinaanza leo Jumatatu. Mkutano huo, umeitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unahudhuriwa na viongozi wa nchi 47 kutoka Afrika.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao kuacha kupoteza muda kujadili mambo yasiyokuwa na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika kujenga hoja yenye nguvu zaidi ya uraia pacha, jambo ambalo ni moja ya mambo yatakayojadiliwa katika mchakato wa Katiba mpya.
“Mnashinda kwenye blogu mkijadili mambo ambayo wenzenu nyumbani wana uwezo mkubwa zaidi kuyajadili kuliko nyie. Mnajiingiza katika mambo ambayo sisi nyumbani tuna uwezo mkubwa nayo kuliko nyie. Kwa mambo haya, sisi tunatosha zaidi. Mnaacha kujadili mambo yanayohusu maisha yenu – kama hili la uraia pacha na mnajiingiza katika mambo yasiyowahusu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa sasa upo huu mjadala wa uraia pacha ni hoja yenu. Nyie badala ya kushiriki katika mjadala huu kwa njia zote, mnashinda kujadili mambo ambayo hayana maana. Kwanza hoja ya uraia pacha siyo hoja ya watu wengi nyumbani, siyo jambo linalowahusu. Hata rasimu sina uhakika kama mmeisoma vizuri na kujua nini kimependekezwa – lakini hata huo muda hamna. Kazi yenu mnashinda mnajadili mambo yasiyokuwa na maana – nani kavaa nguo fupi, nani kafanya nini, haya ndiyo mambo yanayochukua muda wetu.”
Rais Kikwete amesisitiza: “Ushauri wangu ni kwamba tumieni muda wetu kusaidia kusukuma hoja yenu hii muhimu – ambayo kama mnavyojua imeingizwa katika rasimu kwa mapendekezo ya CCM kwa sababu suala hilo halikuwemo katika rasimu ya kwanza.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti, 2014. 
Source Peter Ligate- Facebook

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment