Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome akifafanua jamb wakat iwa hafla fupi ya kusaini mkataba
Na: Rose Masaka – MAELEZO
Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu wa shilingi bilioni 203 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu katika mpango wake wa matokeo makubwa sasa(BRN).
Mkataba huo umesainiwa na Katibu mkuu wa wizara ya fedha Dk. Servacus Likwelile huku ukiwashirikisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elinu na Naibu Katibu Mkuu kutoka TAMISEMI leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya kusaini mkataba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacus Likwelile ameishukuru Benki ya Dunia kutoa mchango huo kusaidia sekta ya elimu nchini na kuwataka TAMISEMI na Wizara ya Elimu kusimamia vizuri pesa hizo ili kuleta mafanikio zaidi kufikia malengo ya matokeo makubwa sasa.
Aidha Dk. Likwelile amewataka waajiri wote katika sekta ya elimu kutoa kipaumbele kwa walimu ili waweze kuboresha elimu nchini na kuwataka kupeleka majina na akaunti namba za walimu wote Hazina ili Hazina iweze kuwawekea mishahara yao katika akaunti zao kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome amesema kuwa Wizara ya Elimu kwa sasa imepiga hatua kubwa katika kufanikisha lengo la matokeo makubwa sasa linalolenga kukuza na kuendeleza elimu katika ngazi ya shule za msingi na sekondari hivyo fedha hizo zinatumika kutatua matatizo katika sekta ya elimu ambapo kwa sasa shule nyingi zimeanza kuonesha matokeo mazuri.
Akitoa mchango wake wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Philippe Dongier amesema kuwa Benki ya Dunia imeona kuna umuhimu wa kuisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ili kuleta ujuzi na kuvumbua vipaji kwa vijana wadogo watakaosaidia kuleta maendeleo hapo baadae.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI Dk. Deo Mtasiwa ameahidi kusimamia fedha hizo kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa zinawafikia walengwa wote hadi ngazi ya chini waweze kufaidika na pesa hizo.
0 comments :
Post a Comment