NA RAYMOND MINJA IRINGA.
KIONGOZI wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amezitikisa ngome za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa kwa kuzoa wanachama wapya zaidi ya 1,000 katika wilaya za Mufindi, Iringa Vijijini na Manispaa ya Iringa.
Wakati CCM inajivunia kuwa na ngome nzito katika wilaya za Mufindi, Iringa Vijijini na Kilolo, kwa upande wao Chadema wanajivunia ngome yao katika jimbo la Iringa Mjini wanaloliongoza kupitia mbunge wake, Mchungaji Peter Msigwa.
Kabwe na viongozi wenzake wa chama hicho kinachojinasibu kupigania uzalendo, juzi walikuwepo mkoani Iringa na kufanya mikutano Mafinga Mjini wilayani Mufindi, Ifunda Iringa Vijijini na Mwembetogwa mjini Iringa; mikutano iliyohudhuriwa na mamia ya watu wa maeneo hayo.
Mikutano hiyo kwa mujibu wa viongozi hao ililenga kukitangaza chama hicho na kunadi sera zake kinapoendelea kujipanga kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao.
Tofauti na vyama vingine vinavyouza kadi zake katika mikutano yake jukwaani bila kuwafanyia usajili wanachama wapya, katika mikutano ACT wazalendo, makada wa chama hicho walikuwa wakiuza kadi na kuwasajili wanachama wao wapya katika madaftari yao ya wanachama.
Pamoja na kuwasajili, wanachama hao wapya walikutanishwa baada ya mikutano hiyo na kufanyiwa semina fupi kuhusu mambo mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya chama hicho.
“Nawashukuru sana kwa kuja kwenye mikutano yetu; tumewaletea chama kipya, kitakachokuwa na siasa tofauti na za vyama vingine, kitakachofanya siasa za masuala ya wanachi na wala sio za watu; hamtatusikia sisi tukimtukana mtu wala tukitukana chama kingine,” alisema.
“Tunataka sauti za wakulima, wafugaji, walimu, manesi, wafanyakazi, madereva, wasukuma mikokoteni, mama ntilie, vibarua, wanaopinga ubinafsishaji wa ovyo, na wanyonge wote Tanzania zisikike,” alisema na kuongeza kwamba hiyo ndio tofauti yao na vyama vingine vinavyotaka sauti za wakubwa na viongozi wao zisikike.
Mishahara ya wabunge
Katika mikutano hiyo Kabwe alikumbusha ajenda ya kilichokuwa chama chake cha Chadema ya kupinga malipo makubwa wanayopata wabunge wakati wa kampeni zake za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
“Jamani wabunge wa nchi hii wanalipwa sana, mbunge akiingia bungeni asubuhi, akitoka mfukoni anaingiza Sh 330,000 ambazo ni zaidi ya mshahara wa mwezi mzima wa nesi, mwalimu na polisi anayeanza kazi,” alisema.
Huku akishangiliwa mara kwa mara katika mikutano hiyo, Kabwe alisema mwaka 2011 yeye na wabunge wenzake hao walikubaliana waikatae posho hiyo ili kurudisha misingi muhimu ya Taifa, lakini wenzake wakamsaliti na kuendelea kuichukua huku yeye pekee akiikataa.
Kuhusu kurejesha Azimio la Arusha
Kabwe alisema; “wapo watu wanabeza wakisema haiwezekani kurejesha azimio la Arusha kwasababu msingi wake mkuu ulikuwa ujamaa; ujamaa tunaouzungumza hapa ni ujamaa utakaoleta uzalendo na ukombozi.”
Alisema ACT itatumia mambo makubwa manne katika azimio hilo kuhamasisha uzalendo na ukombozi wa kweli wa mtanzania.
“Mambo hayo manne ni siasa ya ukombozi, siasa ya kujitegemea inayotoa majibu ya tofauti ya kimaendeleo kati ya mijini na vijijini, madhumuni ya chama na miiko ya uongozi,” alisema.
Kuhusu miiko ya uongozi alisema ACT imeanza kutekeleza kwa kuweka kifungu katika katiba yake kinachowataka viongozi wake wote watangaze mali, madeni na maslai yao kama wanadhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi katika Taifa lao.
“Ifikapo Juni 30, 2015 lazima viongozi wote wa Act tuwe tumeweka hadharani mali na madeni yetu. Ni hatua muhimu sana katika kujenga taifa ambalo halina ufisadi na viongozi wanaotumia madaraka yao kunyonya wananchi; wito wangu viongozi wengine wafanye hivyo sasa,” alisema.
Kabwe alisema ukiwa upinzani ni rahisi sana kujinadi hadharani kuupinga na kuuchukia ufisadi na kufuata miiko ya uongozi na kama hivyo ndivyo ni muhimu viongozi wake wakafanya hivyo sasa kwa kutangaza mali, madeni na maslai yao.
“Najua kuna propaganda nyingi zinaendelea dhidi yangu; watu wa Iringa nipimeni kwa matendo yangu, msinipime kwa maneno ya wapinzani wangu, wekeni rekodi za wabunge wote hadharani, mtapata jibu ni nani mnyonge mwenzenu na ni nani anawatetea,” alisema.
Mwenyekiti wa ACT- Tanzania, Anna Mughwira
Aliwakumbusha watu wa mkoa wa Iringa historia ya Chifu wa wahehe, Chifu Mkwawa na jinsi alivyokuwa mzalendo kwa kujitoa muhanga kupambana na wakoloni ili kulinda maslai ya watu wake.
Mughwira alisema ACT inataka kurejesha misingi ya Taifa inayoendelea kuporomoka kama mafuriko kwasababu ya kutoweka kwa uzalendo.
“Kwahiyo tunataka kuchambua mambo yote mazuri yaliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere na kuyaendeleza katika misingi ya usawa, utu na kusaidiana kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, ”alisema.
Mwigamba na Umasikini
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba, alisema hali ya umaskini nchini imezidi kuongezeka huku viongozi wakiendelea kuponda maisha.
“Wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005 hali ilikuwa mbaya, lakini bado watu walikuwa na matumaini ya kurekebishiwa hali zao, leo anakaribia kumaliza kipindi chake cha uongozi, uchumi bado unamilikiwa na watu wachache.
“Tanzania ni nchi pekee inayochimba madini ya tanzanite, mazao yao Mirerani ni madini, lakini bado Serikali ilichukua ule mgodi na kuwapa makaburu kutoka Afrika Kusini huku Watanzania wakibaki watazamaji. Pia walikuwa wakichimba huku wakiweka maji yenye sumu huku Watanzania wakiendelea kufa kwa Ukimwi na njaa,” alisema Mwigamba.
Alisema pamoja na tanzanite kuchimbwa nchini, lakini nchi ya Afrika Kusini imekuwa ya kwanza katika soko la dunia kwa kuuza madini hayo ikifuatiwa na Kenya huku Tanzania ikishika nafasi ya tisa.
0 comments :
Post a Comment