Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Ujumbe kutoka Uingereza uliotembelea Wizarani hivi karibuni. Kulia kwa Katibu Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu, Ngosi Mwihava. Walioketi upande wa kulia ni Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Kristie Smith (wa kwanza) akifuatiwa na Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose.
- Wahamasisha Serikali kujiunga na Mkakati unaosimamia sekta husika
- Maswi asema kipaumbele ni maslahi kwa nchi; Watanzania
Na Veronica Simba – Dar es Salaam.
Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Kristie Smith amekutana na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini hapa nchini na kufanya mazungumzo yaliyolenga kutambulisha Mkakati wa kimataifa unaosimamia usalama na haki za binadamu katika sekta za mafuta, gesi na madini.
Smith, aliyeongozana na Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose pamoja na Maafisa wengine wawili kutoka Ubalozi huo, alisema ni jambo la busara kwa Tanzania kujiunga na kuwa Mwanachama wa Mkakati huo ili kujenga mazingira mazuri ya usimamizi wa rasilimali husika hususan katika masuala yanayohusu usalama na haki za binadamu.
Alisema kwamba, Mkakati huo unaofahamika kama ‘Voluntary Principles on Security and Human Rights’ ikimaanisha ‘Kanuni za Hiari za Usalama na Haki za Binadamu,’ ulianzishwa mwaka 2000 na unajumuisha wadau mbalimbali ikiwa ni Serikali, Makampuni na Mashirika yasiyo ya kiserikali, unaohamasisha kufuata kanuni maalum zinazozingatia haki za binadamu katika utekelezaji wa shughuli za makampuni ya mafuta, gesi na madini.
Naye Balozi Melrose alisema Tanzania ni nchi muafaka inayopaswa kujiunga na Mkakati huo kutokana na kuwa miongoni mwa nchi zilizojaaliwa utajiri wa rasilimali za mafuta, gesi na madini na hivyo kuwa mwanachama wa Mkakati husika kutaisaidia Serikali kusimamia vema sekta hizo na kuvutia zaidi wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Akijibu hoja zilizowasilishwa na Ujumbe huo kutoka Serikali ya Uingereza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alisema Wizara imepokea ushauri na maombi husika na kwamba itaridhia maombi hayo endapo tu itajiridhisha pasipo shaka kuwa watanzania watanufaika ipasavyo kwa nchi kuwa mwanachama wa Mkakati huo.
“Kama Serikali, tunahitaji muda ili wataalamu wetu wakae na kuchanganua faida ambazo nchi yetu itapata kwa kujiunga na Mkakati huo,” alisema Maswi na kusisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wananufaika, hivyo endapo kutadhihirika kuwepo manufaa ya kujiunga na Mkakati huo, serikali itaridhia.
Akizungumzia zaidi kuhusu umuhimu wa Serikali kujiridhisha kwanza kuhusu faida za kujiunga na Mkakati huo, Katibu Mkuu Maswi alisema tayari Tanzania ni mwanachama wa Mpango wa Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta (Extractive Industry Transparency Initiative – EITI), ambayo malengo yake hayana tofauti kubwa na yale ya Mkakati ulioelezwa.
“Ni vema tupate muda wa kuchambua kwa kina na kujiridhisha kuwa kweli kuna uhitaji wa nchi kujiunga na Mkakati husika kwani pamoja na sababu nyingine, tayari sisi ni wanachama wa EITI,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava aliunga mkono maelezo ya Katibu Mkuu Maswi na kuongeza kuwa ni vema Tanzania ikapata muda wa kuona nchi za kiafrika ambazo tayari ni wanachama wa Mkakati husika kama Ghana ili kujiridhisha zaidi na manufaa yake.
0 comments :
Post a Comment