Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 25, 2014.
ULINZI na usalama watakaowekewa magwiji wa Real Madrid, maarufu kama `Real Madrid Legends` mara watakapowasili jijini Dar es salaam, utakuwa wa hali ya juu na serikali imeahidi kufanikisha hilo kwa asilimia 100.
Nyota waliotikisa soka la dunia wakiwa na Real Madrid na kushinda mataji ya La Liga, UEFA na wengine kushinda kombe la dunia na nchi zao watatua nchini Agosti 22 na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya kikosi maalumu cha nyota wa Tanzania, Agosti 23 uwanja wa Taifa.
Kwa mara ya kwanza barani Afrika Magwiji wa Real Madrid kama vile Luis Madeil Figo, Zinadine Zidane, Fabio Cannavaro, Ronaldo De Lima, Roberto Carlos, Michael Owen watazuru Tanzania na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Saidy Mecky Sadick jana ofsini kwake maeneo ya Ilala jijini Dar, alikutana na kamati ya maandalizi ya ziara hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake, Farough Baghozah na kuelezwa kila kitu.
“Nimekutana nao, wamekuja kunipa maelezo kuhusu ziara hiyo. Dar es salaam kama wenyeji, kuna mambo wanaomba tuwasaidie, moja kubwa ni ulinzi na usalama wakati wote wakapokuwepo Dar”.
“Sisi kama serikali tunawahakikishia kuwa kutakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha kwa siku zote ambazo wachezaji hao watakuwepo Dar”.
“Vilevile kwasababu ziara hii ina lengo la kuutangaza utalii , tutashirikisha na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na bodi ya utalii ili kutumia fursa hiyo”.
“Pia ina faida kwenye michezo, sisi kama serikali tutawasiliana na Wizara ya Habari, Vijana, utamaduni na michezo ili kutumia fursa hiyo”.
“Dar es salaam ipo tayari kuwapokea na tunawasubiri kwa hamu akina Figo”.
“Tunapenda kuwahamasisha kabisa, wajitokeze kwa wingi kwasababu wamejifunza mengi kutoka kwa watu hawa na wenzetu hawa walikuwa sehemu ya watu wanaong`ara zaidi katika mchezo wa soka”. Alihitimisha Mheshimiwa ‘Rais wa Dar’.
Vodacom Tanzania ni miongoni mwa makampuni yaliyojitokeza kudhamini ziara hiyo. Makampuni mengine ni Fastjet, Tropical, Pembe Flower, Lake Gas, EFM Radio na Ladger Plaza Bahari Beach.
Hata hivyo nafasi ya kudhamini bado ipo, waratibu wa ziara hiyo wanatoa wito kwa makampuni na taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini kwasababu ni fursa kubwa ya kujitangaza kitaifa na kimataifa.
0 comments :
Post a Comment