KANUNI ZA KUTOZA FAINI PAPO KWA PAPO USALAMA BARABARANI ZIMESHATAYARISHWA

                                               
                                             Na Abdulla Ali Maelezo- Zanzibar.
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshatayarisha kanuni za usalama wa barabarani za kutoza faini za papo kwa papo kama ilivyo sasa kwa upande wa Tanzania Bara.

Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ali Salum Haji.

Waziri Mohamed amesema kuwa kanuni za sheria ya usalama barabarani kwa upande wa Zanzibar zipo kwa Mwanasheria Mkuu kwa hatua za mwisho na zitaanza kutumiwa na Jeshi la Polisi mara baada ya kukamilika rasmi kwa kutoza faini ya papo kwa papo kwa wote watakaofanya makosa ya usalama wa barabarani.

Waziri Aboud ametanabahisha kuwa kwa sasa Zanzibar Sheria Nambari 7 ya Mwaka 2003 (R.E 2006) ndio inayosimamia masuala ya usalama barabarani na kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu namabari 180 hadi 184 vimeelezea kuhusiana na utaratibu wa faini ya papo kwa papo kwa vyombo vya moto vinavyovunja sheria za usalama wa barabarani Nchini.

Aidha amesema Jeshi la Polisi lina jukumu la kusimamia na kutekeleza Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambapo kwa upande wa Tanzania Bara Sheria inayohusika na usalama wa barabarani ni Sheria nambari 168 ya Mwaka 2002.

“Miongoni mwa majukumu ya Jeshi la Polisi ni kusimamia na kutekeleza Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar”, alieleza waziri Mohamed.

Hivyo ameeleza kuwa kupitia Sheria hiyo Jeshi la Polisi hutekeleza sheria za faini ya papo kwa papo kwa vyombo vya moto vinavyovunja sheria za usalama barabarani na kusaidia Serikali kukusanya fedha nyingi zinazotokana na makosa hayo.

Jeshi la polisi ni Jeshi la Jamhuri ya muungano wa Tanzania na limeundwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 chini ya ibara ya 147 ya kuanzishwa kisheria chini ya kifungu nambari 3 cha sheria ya polisi na polisi wasaidizi Cap.322 R.E ya mwaka 2002.

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment