Vijana kutoka kikundi cha Tunza Mazingira wanaojishughulisha na upandaji wa miche ya miti Wilayani Mwanga wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Afisa vijana Bi. Amina Sanga (wapili kulia) walipotembelewa kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya mradi wao. Kushoto ni Mwezeshaji wa Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa.
Kijana Musa Mchomvu akionyesha mfano wa andiko la mradi wa kikundi chake kijulikanacho kwa jina la Umoja ni Nguvu litakavyokuwa wakati wa semina ya uhamasishaji kwa vijana iliyotolewa na maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana leo Mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Mwanga.
Maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Wanakikundi cha Mwayo Net wakiangalia baadhi ya matofali yaliyofyatuliwa kwa kutumia mashine inayotumia udongo saruji wakati wa ziara ya kutembelea vikundi vya vijana Wilayani Mwanga.
Afisa Vijana Bi. Amina Sanga akiangalia moja ya mashine ya kufyatua matofali kwa kutumia udongo saruji walipotembelea kikundi cha Vijana cha Mwayo Net kinachojishughulisha na ufyatuaji wa matofali Mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Mwanga.
………………………………………………………………..
Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Tarehe: 09/01/2015
Vijana wa Mkoa wa Kilimanjaro wamewataka vijana wenzao kutokuwa na mtazamo hafifu unaowafanya kujenga fikra mbaya kati yao hivyo kushindwa kushirikiana katika kuendeleza mafanikio ya vijana katika mkoa wa Kilimanjaro.
Tarehe: 09/01/2015
Vijana wa Mkoa wa Kilimanjaro wamewataka vijana wenzao kutokuwa na mtazamo hafifu unaowafanya kujenga fikra mbaya kati yao hivyo kushindwa kushirikiana katika kuendeleza mafanikio ya vijana katika mkoa wa Kilimanjaro.
Rai hiyo imetolewa leo na vijana walioshiriki semina inayoendeshwa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwaelimisha vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ujuzi pamoja na stadi za maisha.
Akizungumza wakati wa semina hiyo kijana Musa Mchomvu kutoka kikundi cha Umoja ni Nguvu amesema kuwa mtazamo wa vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulikua ni mdogo sana kutokana na vijana kutokuwa na elimu na uelewa wa kutosha hivyo kuwashukuru wawezeshaji waliotoa mafunzo juu ya mfuko huo na kuwataka vijana wazidi kushiriki semina zinazotolewa kwa vijana ili waweze kupata mwanga utakaowawezesha kujiendeleza.
Kwa upande wake Bibi. Salome Sichalwe amewataka vijana wa Mwanga kuweka siasa pembeni kwa kuachana na ahadi zinazotolewa na wanasiasa wanaowasababishia vijana kubweteka bali wajiwekee malengo yatakayowawezesha kuunda Saccoss imara ya Wilaya na kujiunga katika vikundi vya ujasiliamari kwa maendeleo ya Wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Naye Bw. Idrisa Bajah wa kikundi cha Mwanga Youth Employment Fund amesema kuwa Wilaya ya Mwanga imekua na changamoto ya ajira kwa vijana lakini kutokana na semina waliyoipata itawasaidia vijana walioudhuria kuwanusuru vijana wenzao walioko mitaani kwa kuwapatia njia mbadala za kiujasiriamali.
Aidha mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa amesema kuwa vijana wengi wamekata tamaa kwasababu hawajitambui, hawatambui fursa zinazowazunguka na kukosa ubunifu kitu ambacho kinachowafanya kushindwa kutumia rasilimali ndogo zilizopo kujiendeleza.
Bibi. Riwa amezitaka Halmashauri kutekeleza mwongozo wa kuwasaidia vijana kupata mkopo unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kuunda Saccoss za Wilaya, kusimamia utengenezaji wa vikundi hai vya vijana na kuwaongoza vijana kuandika miradi iliyo na mashiko ili kufanikisha zoezi la kupatiwa mikopo inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kurejesha mikopo hiyo katika mfuko kwa ajili ya kupatiwa vijana wengine wanaohitaji mkopo.
0 comments :
Post a Comment