MIMBA, UTORO KYELA VYAMTISHA WAZIRI MKUU

Waziri  Mkuu, Mizengo Pinda  na mkewe Tunu (wapili kulia) akitazama mafunzo kwa vitendo wakati alipokagua maabara ya Kemia katika shule ya seondari ya Mwaya wilayani Kyela Februari 26, 2015.
                                                                                 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwasaka na kuwakamata wale
wote waliowapa ujauzito wanafunzi na kuwafikisha mahakamani mara moja
ili liwe fundisho kwa wengine.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye shule ya sekondari ya Mwaya,
kwenye kata za Ikusya na Lusungo na wakazi wa mji wa Kyela, jana
(Jumatano, Februari 26, 2015), Waziri Mkuu alisema elimu ni jambo la
msingi sana kwa kizazi cha sasa na kijacho na Serikali haiwezi kuona
fursa za elimu zikichezewa kiasi hicho.
“Haiwezekani hata kidogo! Serikali hatuwezi kuwa tunahimiza ujenzi wa
madarasa kila kukicha halafu watoto wanaopaswa kusoma kwenye hizo
shule wao wanatoroka. Hawa watoto wana wazazi, iweje kuwe na utoro
kiasi hiki?” alihoji.
“DED na DC wabaneni wazazi na mabinti walioharibiwa masomo, ni lazima
watawataja wanaume waliohusika kuwapa mimba. Kwa kuanzia anzeni na hao
wa mwaka jana ambao ni wasichana 11. Wakiwekwa ndani wachahe itakuwa
fundisho kwa wengine,” alisema.
Akielezea ukubwa wa wa tatizo hilo kwenye shule za sekondari peke
yake, Waziri Mkuu alisema mwaka 2010, wasichana 26 walipewa ujauzito;
mwaka 2011 (wasichana 22); mwaka 2012 (wasichana 19); mwaka 2013
(wasichana 16) na mwaka 2014 (wasichana 11). “Jumla yao ni 94, hii ni
idadi kubwa sana. Akina baba waacheni watoto hawa wamalize masomo,
msiwaharibie maisha,” alikemea.
Akichanganua takwimu za utoro kwa wanafunzi haohao wa sekondari,
Waziri Mkuu alisema mwaka 2010 walitoroka wanafunzi 95; mwaka 2011
(wanafunzi 160); mwaka 2012 (wanafunzi 212); mwaka 2013 (wanafunzi 90)
na mwaka 2014 (wanafunzi 88).
“Katika kipindi cha miaka mitano, jumla yao wote hawa ni 645. Hali hii
haivumiliki na jambo liko ndani ya uwezo wa Halmashauri yenu.
Fuatilieni wazazi wa hawa watoto na DC na DED ni lazima tabia hii
ikomeshwe mara moja,” alionya.

Aliwaasa watoto wa wilaya wawe makini na masomo na waache tabia ya
utoro na kupenda mambo ya maisha. “Wanangu someni kwa bidii, achaneni
na haya mambo mengine. Ukipoteza nafasi masomo kidato cha tatu au cha
nne, maisha yako yanakuwa yameharibika,” aliwaasa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwageukia wanaume wanaowafuata watoto wa
shule na kuwataka kimapenzi wakati wanawake wa wilaya ni wengi kuliko
wanaume. “Wlaya hii ina wanaume 106,012 na wanawake 115,478. Sasa ni
kwa nini msiwafuate hao akinamama wakubwa ambao ni wengi kuliko ninyi?
Acheni huo mchezo, waacheni hawa watoto wa kike wamalize masomo yao,”
alisisitiza.
Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Kyela,
Bi. Margareth Malenga alisema kushamiri kwa biashara kwenye mpaka wa
Kasumulu, mkoani Mbeya, kumechochea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi
wanaotoroka shuleni na kwenda kujishughulisha na biashara ndogondogo
mpakani hapo.
“Aidha, kukosekana kwa chakula kwenye baadhi ya shule za msingi na
sekondari wilayani hamu, ni sababu nyingine inayofanya wanafunzi
waache masomo na kwenda kufanya biashara ndogondogo kwenye mpaka wa
Kasumulu,” aliongeza.
Alisema hali hiyo imechangiwa na kuwepo kwa baadhi ya kaya masikini
zinazoshindwa kuwalipia gharama za masomo watoto wao.
Akifafanua, Bi. Malenga alisema katika kipindi cha mwaka 2012 hadi
2014, wavulana 414 na wasichana 159 waliochaguliwa kujiunga na elimu
ya sekondari waliacha shule kwa sababu za utoro.
Kuhusu elimu ya msingi, Bi. Malenga alisema, wanafunzi wapatao 711
wametoroka shule lakini kutokana na jitihada zilizofanyika, wanafunzi
155 wamerudishwa shuleni. “Wanafunzi 556 waliobakia wanaendelea
kutafutwa kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji ili waweze
kuwarudishwa kuendelea na masomo,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wameanzisha utaratibu wa kila Mkuu wa
Shule kuwasilisha ripoti ya mahudhurio ya wanafunzi kwa watendaji wa
kata na vijiji kila Ijumaa ambapo tangu utaratibu huo uanze,
wamefanikiwa kudhibiti utoro kwa asilimia 91.

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment