Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) juu ya mafanikio ya uzalishaji wa chakula nchini kwenye viwanja vya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) jijini Dar es Salaam.
Hussein Makame-MAELEZO
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza amesema kuwa kwa sasa Serikali iko kwenye mikakati kujenga maeneo ya kuhifadhia mazao ya wakulima baada ya utoshelevu wa chakula kufikia asilimia 124 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula nchini.
Mhandisi Chiza aliyasema hayo leo wakati akizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uzalishaji wa chakula nchini na mikakati ya Serikali ya kumkomboa mkulima kutokana na nguvu anayoitoa katika shughuli za kilimo.
Alisema kwa mwaka 2011 hadi 2012 uteshelevu wa chakula katika nchi ulifikia asilimia 111 ya mahitaji, wakati mwaka 2012 hadi 2013 uteshelevu ulifikia asilimia 112 huku mwaka 2013 hadi 2014 uteshelevu ulifikia asilimia 118.
Waziri Mhandisi Chiza alifafanua kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya wakulima kuhamasishwa kuzalisha zaidi kwani miaka kadhaa iliyopita Serikali iliweka marufuku ya kutouza mazao nje kutokana na uhaba wa chakula.
“Miaka iliyopita tuliweka marufuku ya kutouza mazao nje lakini hilo sio suluhisho na suluhu ni kuzalisha zaidi, hivyo tumeendelea kuzalisha mazao hususani ya chakula kwa kasi, hatuna budi kuwapongeza wakulima kwa kufanya kazi kubwa” alisema Waziri Mhandisi Chiza.
Alisema kuongezeka kwa utoshelevu wa chakula nchini kumechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kutoa maeneo zaidi kwa shughuli za kilimo, kuongezeka kwa matumizi ya mbolea, matumizi ya mbegu bora na kuongeza maeneo ya umwagiliaji.
Hata hivyo, Waziri Mhandisi Chiza alisema baada ya kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula, changamoto iliyopo ni kutafuta masoko ya mazao hayo ambapo Serikali imechukua hatua mbalimbali na kuwaruhusu wakulima kuuuza mazao yao nje.
“Serikali imeanza kuwatafutia wakulima masoko ya nje, tulikwenda Kenya na Sudan Kusini ambapo mazao ya wakulima wa Tanzania yanahitajika kwa wingi ikiwemo mchele, mahindi, vitunguu” alisema Waziri Mhandisi Chiza na kuongeza kuwa:
“Pamoja na hivyo, naomba wadau wa kilimo watusaidie katika masuala ya biashara na masoko na sisi Serikali kazi yetu ni kusawazisha changamoto za bei, usalama na ulanguzi kwani lengo ni kumsaidia mkulima apate faidi ya nguvu anayoitoa katika kilimo”
Alisisitiza pamoja na juhudi hizo kwa sasa Serikali iko kwenye mkakati wa kujenga maeneo ya kuhifadhi mazao ya wakulima ambapo inatarajia kutumia Dola za Kimarekani Milioni 50 kwenye maeneo ya kimkakati.
“Hata sasa Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) wako kwenye mkakati wa kupata fedha kutoka benki ya CRDB kununua mazao ya wakulima na kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kuvuka uwezo wa sasa wamaghala yake kuhifadhi tani 200,000 za chakula” alisema Waziri Mhandisi Chiza.
Alibainisha kuwa ili wakulima wa Tanzania wafaidike ni lazima taratibu za masuala ya mazao zizingatiwe na iwapo mkulima atakuwa na shida yoyote anatakiwa kuishirikisha NFRA
Pia aliwataka wafanyabiashara binafsi waache kuwalangua wakulima kwa kuwafuata mashambani huku akiomba wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya shilingi 500 kwa kilo huku akiwasisitizia viongozi wa mikoa, wilaya, kata na vijiji washirikiane na wakulima na kutatua changamoto zinazowakabili.
Baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) na waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza, akiangalia magunia ya vyakula yaliyohifadhi wa kwenye ghala la Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) baada ya kuzungumza na waadhishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza, akitoa ufafanuzi kwa mmoja wa waandishi wa habari kabla ya kuondoka kwenye viwanja vya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA).Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) Charles Walwa.
0 comments :
Post a Comment