Benjamin Bizele mmoja wa maofisa kutoka kampuni ya simu ya TTCL akishusha vyakula hivyo huku muugumzi mkuu wa hospitali hiyo Mary Haule akivipokea.
Muuguzi Mkuu wa hospitali ya Ocean Road Mary Haule akitoa shukurani zake kwa kampuni ya simu ya TTCL kwa msaada ilioutoa kwa wagonjwa wa hospitali hiyo.
………………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Wagonjwa wa saratani wa mikoani sasa watapata matibabu ya ugonjwa huo kwa njia ya mtandao baada ya kampuni ya simu Tanzania (TTCL kuzindua huduma ijulikanayo kwa jina la Afya Mtandao ambayo itamwezesha mgonjwa kupata huduma akiwa katika moja ya hospitali ya rufaa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada ya vyakula kwa Taasisi ya Kansa ya Ocean Road jana, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa wateja cha TTCL, Laibu Leonard alisema kuwa kupitia kwa Afya-Mtandao ambayo inatumia mkongo wa taifa wa mawasiliano, madaktari wa Taasisi ya Ocean Road wataweza kuendesha huduma mbalimbali za matibabu pamoja na upasuaji huku wakiwa katika chumba maalum ambacho kitawawezesha kuona na kutoa mtazamo wa wa zoezi la upasuaji linaloendelea mikoani.
Laibu alisema kuwa hata huduma ya mionzi itafanyika kwa kushirikisha madaktari bingwa waliounganishwa na huduma hiyo ambayo ni ya kisasa zaidi. Alifafanua kuwa mbali ya mikoani, tiba hiyo inaweza kufanywa hata kwa kushirikisha hospitali kubwa za nchi mbalimbali na hivyo kupunguza gharama kubwa za matibabu.
“Hakuna haja ya kwenda India, Uingereza, Ujerumani na nchi nyingine kwa ajili ya upasuaji au huduma nyingine za tiba, unaweza kufanyiwa upasuaji Bugando, madaktari wa Ocean Road, KCMC, Tumbi, Temeke, Mwanyamala na nchi ya Tanzania wataona na kushiriki ipasavyo katika tiba hiyo, hii inatokana na kuunganishwa kwa mtandao ambao utaonyesha picha za video, za kawaida na huduma ya sauti,” alisema Leonard.
Alisema kuwa lengo la TTCL ni kuunganisha hospitali zote za rufaa nchini ifikapo mwezi Machi mwakani ili kuraisisha huduma hiyo. Kuhusiana na msaada wa vyakula wenye thamani ya Sh Milioni 3, Leonard alisema kuwa wameamua kutoa msaada huo ili kupunguza gharama za vyakula kwa wagonjwa ambao wamelazwa katika taasisi hiyo.
0 comments :
Post a Comment