MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA IRINGA AMFIKISHA POLISI MWENYEKITI WAKE WA WILAYA

                                             Bw  Frank Nyalusi  Na Matukiodaimablog
Hali ya  kisiasa  ndani ya  chama  cha Demokrasia na maendeleo (chadema)
mkoa wa Iringa si shwari  baada ya mwenyekiti wake mkoa  wa Iringa
Mustapher Msowela kumfikisha polisi  mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Iringa mjini , Frank Nyalusi.
Nyalusi ambae  pia ni  diwani  wa kata ya Mvinjeni jimbo la Iringa mjini juzi
alitiwa nguvuni na  jeshi la Polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
 
Nyalusi aliyeshitakiwa katika kituo cha Polisi cha kati cha mjini Iringa jana, anatuhumiwa kumtusi mwenyekiti wake huyo wa mkoa kupitia mitandao ya simu; matusi yanayoendelea kuchunguzwa na jeshi hilo.

Nyalusi amekamatwa kwa tuhuma hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya kudaiwa kutoa tuhuma za uongo kwa lengo la kujipatia umaarufu dhidi ya mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa, Salim Asas ambaye pia ni Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Iringa.
 
Katika mkutano wa hadhara uliofanywa na Chadema Desemba 21 kwenye uwanja wa
Mwembetogwa mjini Iringa, Nyalusi ambaye pia ni diwani wa kata ya Mivinjeni
alitoa tuhuma zinazowahusisha vijana watatu ambao hata hivyo hakuwataja majina
kwamba walitumwa na Asas kwenda kumuua.
 
Asas kwa kupitia kwa wakili wake, Alfred Kingwe amekanusha tuhuma hizo alizoziita ni za kipuuzi ambazo haziwezi kubebeka hata kwa mzani mdogo wa kupimia madini.
 
Ili kumsafisha mteja wake, Kingwe alisema ndani ya siku 14 toka akabidhiwe hati ya
madai (Demand Note), Nyalusi anatakiwa kuitisha mkutano katika eneo lile lile
alilotolea tuhuma hizo na kuzikanusha vinginevyo atafikishwa mahakamani.
 
Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema;  “Kuhusu tukio la kumtukana
mwenyekiti wake wa mkoa, Nyalusi alikamatwa jana mara baada ya Msowela
kuwasilisha malalamiko yake polisi, akahojiwa na kuachiwa baada ya kukamilisha
taratibu za dhamana.”
 
Alisema
jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hilo la kijinai na endapo litathibitika
kuwa la kweli, Nyalusi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mivinjeni mjini Iringa
atafikishwa mahakamani.
 
Kuhusu tukio linalomuhusisha na Asas, Kamanda Mungi alisema jeshi la Polisi limefanya mahojiano ya awali na wahusika hao.
 
“Jambo hili lipo, tunachunguza; yapo maneno Nyalusi ameyatamka kwenye mkutano wao wa hadhara kwamba ametishiwa kuuawa, ametumiwa watu watatu kwenda kumuua wakiwa na visu. Kumtishia mtu ni kosa la jinai na kumtuma mtu kwenda kumdhuru mtu mwingine ni kosa la jinai, kwahiyo tunachunguza” alisema.
 
Alisema katika mazingira ya uwazi, Polisi inachunguza suala hilo ili kujua Nyalusi
alitishiwa katika mazingira gani; alitishiwa na nani na kwanini hakwenda kutoa
taarifa hiyo Polisi na kufungua kesi ili Polisi iwakamate wahusika na kulinda maisha
yake.
 
“Lakini tunajaribu kuangalia kama hakutishiwa na ametamka vile katika mkutano wa
hadhara, lengo lake lilikuwa ni nini na kama anajua madhara yake kwa jamii
iliyosikia taarifa hiyo ni yepi,” alisema.
 
Alisema kama itabainika taarifa zilizotolewa na Nyalusi ni za uongo, sheria itachukua
mkondo wake na kama itadhihiri ni za kweli sheria pia itachukua mkondo wake.

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment